May 13, 2016

D.I.A.M.O.N.D Herufi za Jina Zina Siri Nzito

Inawezekana kabisa unatamani uwe kama Diamond Platnumz, kukusanya mkwanja kila siku, kwenda unapopataka na hata kula unachokitaka. Sawa! ... thumbnail 1 summary
Inawezekana kabisa unatamani uwe kama Diamond Platnumz, kukusanya mkwanja kila siku, kwenda unapopataka na hata kula unachokitaka. Sawa! Inawezekana, juhudi zako ndiyo kitu cha msingi sana, si kuwa kama yeye bali unaweza kuwa hata zaidi yake. 


Mbali na usupastaa wake, fedha zake lakini kuna asilimia kubwa Diamond anabebwa na jina lake. Jina lake linamuelezea yeye ni mtu wa aina gani na anahitaji nini. Hebu tufanye kitu kimoja, hilo jina lake, ligawe kwenye herufi mojamoja, utagundua kwamba anafanya vile herufi za jina lake zilivyo.
D (DOMINANT)

Hili ni neno la Kiingereza lenye maana ya ‘mwenye nguvu au mtawala’. Hutakiwi kujiuliza maswali mengi juu ya hili kwa Diamond. Amekuwa msanii mwenye mafanikio makubwa, inawezekana kuliko wote nchini Tanzania.

Alianza kutawala katika redio mbalimbali tangu alipotoa Mbagala na Kamwambie miaka hiyo ya nyuma. Hakuishia hapo, utawala wake umekwenda mpaka sasa hivi anapotamba na wimbo wa Make Me Sing aliopiga na AKA kutoka Afrika Kusini. Ametawala muziki wa Bongo na hivi karibuni anaweza kutawala Afrika nzima, cha msingi ni kumpa muda tu. 

I (INDEFATIGABLE) 
Hili ni neno la Kiingereza lenye maana ya ‘asiyeshindwa au kuchoka’. Diamond amekuwa msanii wa tofauti sana, mara nyingi si mtu anayekubali kushindwa, tuliona kipindi P Square walipotua Bongo na kusema hawamjui Diamond. 
Inawezekana kwa msanii mwingine angeona ndiyo basi tena, ila kwake, hakuchoka, hakukubali kushindwa, alijazatiti na mwisho wa siku, kuna bonge la kolabo linakuja na wasanii hao. Unapoona unataka kushindwa, jua mafanikio yanakaribia. 

A (AMBITIOUS) 
Hili ni neno lingine lenye maana ya ‘mtafuta mafanikio au mambo makubwa’. Tumeliona hilo kwa Diamond, mara nyingi amekuwa mtu wa kutaka kutafuta mambo makubwa, hakuridhika na jinsi Wabongo tunavyofanya, akaangalia njia ya kutusua na mwisho wa siku, yale makubwa aliyoyatafuta, akayapata. 

Yeye akawa njia kubwa ya wasanii wa Kibongo kufanya video mbele. Hajaishia hapo, mlima mmoja tu ndiyo uliobaki, kuutambulisha Muziki wa Bongo Fleva duniani kote. 

M (MELODIUS) 
Hili ni neno lenye maana ya mtu mwenye melodi nzuri. Muziki ni sauti na sauti ndizo zinaufanya muziki kuwa bora. Kama Diamond asingekuwa na sauti nzuri, asingekubalika na watu wanaojua muziki. 
Amepambana, japokuwa kipindi cha nyuma wengi waliongea kuhusu sauti yake, mwisho wa siku akabadilika na kuwa na melodi nzuri tu. Hii imempa nguvu na leo kujikuta yuko juu, akiogelea katika ulimwengu ambao wasanii wengi wa Bongo wanautamani. 

O (OUTCLASS) 
Hili ni neno lenye maana ya ‘bora kuliko’. Ndiyo! Tumeona ni kwa namna gani Diamond alivyowakuta watu katika gemu lakini mwisho wa siku, yeye amekuwa bora kuliko hao aliowakuta. Ameweza kufanya kazi nzuri, kujituma usiku na mchana, kujitangaza na hata pale alipobebwa, alibebeka kikamilifu. Ni mfano wa kuigwa, kama mwanamuziki anatamani kuwa kama Diamond, anatakiwa kuwa na kiu ya kuwa bora. 

N (NEAT) 
Hili ni neno lingine lenye maana ya ‘msafi’. Mwangalie Diamond, kila siku amekuwa msafi kimuonekano wa nje, hakuishia hapo, pia alianzisha lebo yake iitwayo Wasafi, unajua kwa nini? Ni kwa sababu yeye ni msafi. Mwanamuziki unatakiwa kuwa hivyo. 

D (DISCIPLINED) 
Hili hutokana na neno discipline, yaani ni ‘mwenye nidhamu’. Ukimwangalia Diamond utakubaliana nami. Ni mara nyingi amekuwa mtu wa kuzingatia muda, unapomwambia afike sehemu fulani, si mtu wa kuchelewa kama ilivyo kwa wasanii wengine, hasa wanaotafuta majina hapa Bongo. 
Si hapo tu, si mtu wa kumzungumzia mtu kiugomvi, pamoja na jina lake, huwa si mtu anayetafuta kiki kupitia ugomvi ni mtu anayejiheshimu, anaheshimu kazi zake ambazo kila siku zinamfanya kuwa juu.

SHARE THIS POST TO SOCIAL MEDIA BELOW:

No comments