Marehemu Nelson Mandela enzi za uhai wake. Mwandishi Wetu na Mitandao WOSIA aliowahi kuuandika hayati Nelson Rolihlahla Mandela...
11:35
Marehemu Nelson Mandela enzi za uhai wake.
Mwandishi Wetu na Mitandao
WOSIA aliowahi kuuandika hayati Nelson Rolihlahla Mandela ‘Mzee
Madiba’ au ‘Tata’ (95) enzi za uhai wake akielezea anavyotaka azikwe,
ndiyo tishio kubwa lenye utata kuelekea siku ya mazishi yake, Jumapili
ijayo, Ijumaa Wikienda limebaini.
Mtandao mmoja nchini humo
umeukumbushia wosia huo huku familia ikianza kuonesha misimamo
tofautitofauti, hali inayoashiria kuibuka kwa makundi mawili
yanayokinzana.
Gari lililobeba mwili wa Nelson Mandela.
FAMILIA INAVYOTAKA
Habari za ndani zilisema kuwa
familia inataka mazishi ya kiongozi huyo maarufu duniani yawe makubwa
na ya kisasa kwa vile viongozi wa nchi mbalimbali duniani watahudhuria.
“Mandela ni kingozi mkubwa sana duniani, mazishi yake lazima yawe
makubwa pia ya kisasa. Hawezi kuzikwa kama mwananchi wa kawaida,”
ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Mmoja wa waombolezaji akigusa picha na Mandela.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa wakati familia hasa wajukuu na watoto
wake wakishikilia msimamo huo, wapo wanandugu wanaotaka azikwe kama
alivyoandika katika wosia wake huo.
SERIKALI YAPANGA MAMBO BILA KUFUATA WOSIA
Habari
zaidi zilisema kuwa Serikali ya Afrika Kusini inajitahidi kuupangua
wosia huo kwa kuendelea na maandalizi ya mazishi kama haukuwahi kuwepo
licha ya kwamba jamii ya watu nchini humo inaheshimu wosia wa marehemu.
WOSIA UNAVYOSEMA
Mzee Madiba alishauandika wosia
huo kwenye karatasi moja tu ambapo aliagiza anavyotaka azikwe. Alisema
kuwa akifa azikwe katika milima iliyojitenga nyumbani kwa mababu zake
katika Kijiji cha Qunu, Eastern Cape huko ‘Sauzi’.
Waombolezaji wakiweka maua katika sanamu la Mandela.
ALITAKA MAZISHI YA KAWAIDA SANA
Inadaiwa wosia
huo aliuandika Januari, 1996 wakati bado akiwa rais ambao ulijaa
maelekezo yote juu ya mazishi yake. Aliagiza kufanyiwa mazishi ya
kawaida sana yenye hadhi ya raia wa kawaida nchini humo hivyo kuyafanya
kuwa makubwa na ya kifahari ni kukiuka wosia wa mzee.
KABURI ALILOLITAKA MANDELA
Katika wosia wake huo
uliotolewa na rafiki yake wa karibu, Mzee Madiba aliandika kuwa akifa
azikwe katika eneo la familia lenye makaburi ya ukoo wa Mandela kijijini
hapo.
Pia aliagiza kuwa kaburi lake liwekewe jiwe la kawaida kama
alama ya mahali lilipo ili lisije kupotea kwa mvua au mabadiliko ya
tabia nchi.
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma.
KABURI LISISAKAFIWE
Katika tafsiri ya maneno
hayo, Mzee Madiba alitaka kaburi lake liwe la kawaida sana, akimaanisha
lisijengewe kama ilivyokuwa kwa makaburi ya viongozi wengine wa mfano
wake barani Afrika kama, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Kamuzu
Banda (aliyekuwa Rais wa Malawi).
WOSIA WAKE ULIKUWA WA UPANDE MMOJA WA KARATASI
Magazeti ya nchini humo, South African Mail na Guardian miezi ya
karibuni yaliripoti kumnukuu rafiki huyo wa siku nyingi wa familia ya
Mandela akisema: “Madiba hakuwahi kukifanya kifo kuwa jambo kubwa la
kufikiriwa, pia hakuwahi kutaka chochote cha fahari wakati wa kumzika.”
Cha ajabu, wosia huo wa Mandela ulitosha kwenye upande mmoja wa
karatasi ya kawaida ya kuandikia licha ya kwamba mauzo ya kitabu chake
cha Long Walk to Freedom na michoro yenye jina lake vilimpatia mamilioni
ya fedha.
Nelson Mandela (kulia) akiwa na Mwalimu Julius Nyerere enzi za uhai wao.
FAMILIA YACHUKIZWA NA WOSIA
Wosia huo ulielezwa
kuwashangaza watu wengi duniani kwani waliamini angekuwa na vitu vingi
vya kuandika kulingana na uwezo wake.
Kwa mujibu wa Shirika la
Utangazaji la Afrika Kusini, SABC, suala hilo la sehemu atakayozikwa
Mzee Madiba liliiudhi mno familia yake akiwemo yule mjukuu wake ambaye
ni chifu, Mandla Mandela aliyewahi kufikishwa kortini kwa kuhamisha
makaburi hayo ya ukoo na kuyapeleka sehemu nyingine. Pia ndiye msemaji
wa familia ya Mandela.
DUNIA YAMKATALIA
Baadhi ya wanaharakati
ulimwenguni kote walisema wosia huo unapingana na matakwa ya dunia
nzima, ambapo walitaka maziko ya mzee huyo yawe makubwa na ya
kihistoria ambayo hayajawahi kutokea.Ilifahamika kwamba dunia inataka
mazishi hayo yavunje ile rekodi iliyoshikiliwa na mazishi ya Papa John
Paul II aliyefariki dunia Aprili 2, 2005.
Mjukuu wa Nelson Mandela, Mandla Mandela.
SAFARI HII HAKUKIMBIZWA HOSPITALI
Mzee Madiba
ambaye alitimiza umri wa miaka 95 Julai 18, mwaka huu, alikuwa
hospitalini kwa karibu miezi mitatu nyuma akitibiwa maambukizi kwenye
mapafu huku akipumulia mashine. Baadaye alipata nafuu na kurudishwa
nyumbani ambako usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita aliugua ghafla na
kufariki dunia.