June 13, 2014

HABARI NJEMA KWA WALIOAJIRIWA,KODI YA MISHAHARA KUPUNGUA

SERIKALI imepunguza kiwango cha chini cha Kodi ya Mapato ya Mishahara (PAYE) hadi asilimia 12 kutoka asilimia 13. Serikali pia imeahid... thumbnail 1 summary

SERIKALI imepunguza kiwango cha chini
cha Kodi ya Mapato ya Mishahara (PAYE)
hadi asilimia 12 kutoka asilimia 13.
Serikali pia imeahidi kuongeza kima cha
chini cha mishahara, ambacho hata hivyo
hakikutajwa.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum
amelieleza Bunge mjini Dodoma kuwa,

katika Bajeti ya Serikali ya Sh trilioni 19.8,
Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi
na yasiyo ya kodi ya Sh trilioni 12,18, kati ya
hizo, mapato ya kodi ni Sh bilioni 11.31 na
mapato yasiyo ya kodi, ni Sh bilioni 859.8.
Aidha, mapato yanayotokana na vyanzo vya
halmashauri ni Sh bilioni 458.5.
Waziri Mkuya alisema Serikali inaendelea na
jitihada za kupata misaada na mikopo ya
masharti nafuu, ambapo inatarajia kupokea
Sh trilioni 2.94. Kati ya fedha hizo misaada
na mikopo ya kibajeti ni Sh bilioni 922.1,
Mifuko ya Kisekta Sh bilioni 274.1 na miradi
ya maendeleo Sh trilioni 1.75.
Waziri Mkuya alisema kwa nia ya
kuendeleza miradi ya miundombinu nchini,
Serikali itakopa katika soko la ndani Sh
trilioni 3. Kati ya hizo, Sh bilioni 689.56 ni za
kugharimia miradi ya maendeleo na Sh
trilioni 2.3 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani
na dhamana za Serikali zinazoiva.
Pia itakopa Sh trilioni 1.3 kutoka masoko ya
fedha ya nje kwa masharti ya kibiashara
kwa ajili ya kugharimia miradi ya
maendeleo.
Akizungumzia mgawanyo wa fedha, Mkuya
alitaja Sekta ya Elimu kuwa ndiyo
iliyotengewa fedha nyingi kuliko sekta
yoyote katika sekta za kipaumbele
zilizoteuliwa katika Mpango wa Tekeleza
kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Sekta hiyo kwa mujibu wa Mkuya,
imetengewa Sh trilioni 3.466, ambapo kati
ya hizo Sh bilioni 307.3 zimetengwa
kugharimia mikopo ya elimu ya juu.
Fedha zilizobakia zimepangwa kutumika
kuimarisha ubora wa elimu ikijumuisha
miundombinu ya elimu, ambapo Waziri
Mkuya alisema lengo ni kusaidia upatikanaji
wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia,
kuimarisha na kujenga madarasa na
maabara.
Pia Serikali katika sekta hiyo, imekusudia
kuhakikisha vijana wanapata fursa za ajira,
hivyo juhudi zimewekwa kuimarisha vyuo
vya ufundi stadi vilivyo chini ya Mamlaka ya
Elimu ya Ufundi Stadi (VETA).
Sekta ya pili kwa kupewa mgawo mkubwa
ni Miundombinu ya usafirishaji, ambapo Sh
trilioni 2.1 zimetengwa na kati ya hizo, Sh
bilioni 179.0 ni kwa ajili ya ununuzi wa
mabehewa na ukarabati wa Reli ya Kati.
Aidha Waziri Mkuya alisema Sh
trilioni 1.4 ni
kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa
barabara na madaraja.
"Azma hii inalenga kupunguza
msongamano wa magari mijini, gharama za
usafiri na usafirishaji wa bidhaa na
huduma, na hivyo kupunguza mfumuko wa
bei."
Sekta inayofuata kwa kutengewa kitita
kikubwa cha fedha ni Afya, ambayo Waziri
Mkuya alisema Sh trilioni 1.59, zimetengwa
kwa ajili ya ununuzi wa dawa, kuzuia
magonjwa ya mlipuko, chanjo za watoto,
ujenzi wa zahanati na kudhibiti
maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi na
malaria.
Sekta ya Kilimo, imetengewa Sh trilioni 1,08,
kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya
umwagiliaji katika maeneo mbalimbali
yakiwemo ya Ukanda Maalumu wa Kilimo
wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Pia fedha hizo zimelenga kutumika kwa ajili
ya ujenzi wa maghala na masoko; na
upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya kukuza
uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Waziri alisema Serikali itaendelea kuwekeza
kwenye ugani kwa kuimarisha vyuo vya
utafiti katika kilimo na kuhakikisha
kunakuwa na maofisa ugani wa kutosha na
mbegu bora.
"Hatua hii itaimarisha uzalishaji wa mazao,
usalama wa chakula na kuhakikisha
upatikanaji wa masoko ya uhakika,"
alisema.
Kwa upande wa Nishati na Madini, Serikali
imetenga Sh trilioni 1,09, kati ya hizo Sh
bilioni 290.2 zimetengwa kwa ajili ya
Wakala wa Umeme Vijijini (REA), ili
kusambaza umeme vijijini.
Aidha, Sh bilioni 151 zimetengwa kwa ajili
ya kukamilisha ujenzi wa bomba la gesi
kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na Sh
bilioni 90 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi
wa mtambo wa kufua umeme kwa kutumia
gesi wa Kinyerezi I.
"Hatua hii inalenga kuhakikisha upatikanaji
wa umeme wa uhakika na kupunguza
gharama zake na hivyo kuvutia uwekezaji
na kuongeza ajira," alisema.

Sekta ya Maji imetengewa Sh bilioni 665.1
kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya
maji mijini na vijijini ikiwa ni pamoja na
kuendelea na ujenzi wa visima katika vijiji
10 kwa kila halmashauri na kukamilisha
ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu Chini
hadi Dar es Salaam.
Katika Utawala Bora, Serikali imetenga Sh
bilioni 579.4 kwa ajili ya kuimarisha
utawala bora, ikiwa ni pamoja na
kugharimia Bunge Maalumu la Katiba;
vitambulisho vya Taifa; Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa wa mwaka 2014; kuhuisha Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura; maandalizi ya
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015;
mapambano dhidi ya rushwa na utoaji wa
haki kwa wakati.
Katika jitihada za kuongeza mapato zaidi,
Waziri wa Fedha ameondolewa mamlaka ya
kusamehe kodi katika maeneo muhimu,
ambapo Waziri Mkuya aliwaomba wabunge
waiunge mkono Serikali, katika hilo ili
kurahisisha usimamizi wa kodi nchini na
hivyo kutoa unafuu kwa walipa kodi, na
kuongeza mapato ya Serikali.
"Serikali itachukua hatua kuu mbili muhimu.
Kwanza, kutoa taarifa ya misamaha ya kodi
kila robo mwaka kwa kuwatangaza
walionufaika na misamaha kwenye Tovuti
ya Wizara ya Fedha.
"Hatua hii itasaidia kuleta uwazi na
uwajibikaji katika suala la misamaha ya
kodi na kuwafanya wananchi wajue ni nani
anayenufaika na misamaha hiyo," alisema.
Pili, alisema Serikali itatoa taarifa ya kina ya
misamaha yote ya kodi iliyotolewa na
kuiwasilisha bungeni kila mwaka, ili
wabunge mpate nafasi ya kujadili na kutoa
maoni yenu.

SHARE THIS POST TO SOCIAL MEDIA BELOW: