June 13, 2014

HABARI NJEMA KWA WALIO AJIRIWA, KODI YA MISHAHARA KUPUNGUA

SERIKALI imepunguza kiwango cha chini cha Kodi ya Mapato ya Mishahara (PAYE) hadi asilimia 12 kutoka asilimia 13. thumbnail 1 summary

SERIKALI imepunguza kiwango cha chini cha Kodi ya Mapato ya Mishahara (PAYE) hadi asilimia 12 kutoka asilimia 13.

Serikali pia imeahidi kuongeza kima cha chini cha mishahara, ambacho hata hivyo hakikutajwa.

Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum amelieleza Bunge mjini Dodoma kuwa, katika Bajeti ya Serikali ya Sh trilioni 19.8, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya Sh trilioni 12,18, kati ya hizo, mapato ya kodi ni Sh bilioni 11.31 na mapato yasiyo ya kodi, ni Sh bilioni 859.8.

Aidha, mapato yanayotokana na vyanzo vya halmashauri ni Sh bilioni 458.5.

Waziri Mkuya alisema Serikali inaendelea na jitihada za kupata misaada na mikopo ya masharti nafuu, ambapo inatarajia kupokea Sh trilioni 2.94. Kati ya fedha hizo misaada na mikopo ya kibajeti ni Sh bilioni 922.1, Mifuko ya Kisekta Sh bilioni 274.1 na miradi ya maendeleo Sh trilioni 1.75.

Waziri Mkuya alisema kwa nia ya kuendeleza miradi ya miundombinu nchini, Serikali itakopa katika soko la ndani Sh trilioni 3. Kati ya hizo, Sh bilioni 689.56 ni za kugharimia miradi ya maendeleo na Sh trilioni 2.3 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva.

Pia itakopa Sh trilioni 1.3 kutoka masoko ya fedha ya nje kwa masharti ya kibiashara kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo.

Akizungumzia mgawanyo wa fedha, Mkuya alitaja Sekta ya Elimu kuwa ndiyo iliyotengewa fedha nyingi kuliko sekta yoyote katika sekta za kipaumbele zilizoteuliwa katika Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Sekta hiyo kwa mujibu wa Mkuya, imetengewa Sh trilioni 3.466, ambapo kati ya hizo Sh bilioni 307.3 zimetengwa kugharimia mikopo ya elimu ya juu.

Fedha zilizobakia zimepangwa kutumika kuimarisha ubora wa elimu ikijumuisha miundombinu ya elimu, ambapo Waziri Mkuya alisema lengo ni kusaidia upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, kuimarisha na kujenga madarasa na maabara.

Pia Serikali katika sekta hiyo, imekusudia kuhakikisha vijana wanapata fursa za ajira, hivyo juhudi zimewekwa kuimarisha vyuo vya ufundi stadi vilivyo chini ya Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (VETA).

Sekta ya pili kwa kupewa mgawo mkubwa ni Miundombinu ya usafirishaji, ambapo Sh trilioni 2.1 zimetengwa na kati ya hizo, Sh bilioni 179.0 ni kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa na ukarabati wa Reli ya Kati. Aidha Waziri Mkuya alisema Sh trilioni 1.4 ni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja.

“Azma hii inalenga kupunguza msongamano wa magari mijini, gharama za usafiri na usafirishaji wa bidhaa na huduma, na hivyo kupunguza mfumuko wa bei.”

Sekta inayofuata kwa kutengewa kitita kikubwa cha fedha ni Afya, ambayo Waziri Mkuya alisema Sh trilioni 1.59, zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, kuzuia magonjwa ya mlipuko, chanjo za watoto, ujenzi wa zahanati na kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi na malaria.

Sekta ya Kilimo, imetengewa Sh trilioni 1,08, kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya Ukanda Maalumu wa Kilimo wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).

Pia fedha hizo zimelenga kutumika kwa ajili ya ujenzi wa maghala na masoko; na upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya kukuza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

Waziri alisema Serikali itaendelea kuwekeza kwenye ugani kwa kuimarisha vyuo vya utafiti katika kilimo na kuhakikisha kunakuwa na maofisa ugani wa kutosha na mbegu bora.

“Hatua hii itaimarisha uzalishaji wa mazao, usalama wa chakula na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika,” alisema.

Kwa upande wa Nishati na Madini, Serikali imetenga Sh trilioni 1,09, kati ya hizo Sh bilioni 290.2 zimetengwa kwa ajili ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA), ili kusambaza umeme vijijini.

Aidha, Sh bilioni 151 zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na Sh bilioni 90 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa mtambo wa kufua umeme kwa kutumia gesi wa Kinyerezi I.

“Hatua hii inalenga kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kupunguza gharama zake na hivyo kuvutia uwekezaji na kuongeza ajira,” alisema.

Sekta ya Maji imetengewa Sh bilioni 665.1 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maji mijini na vijijini ikiwa ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa visima katika vijiji 10 kwa kila halmashauri na kukamilisha ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu Chini hadi Dar es Salaam.

Katika Utawala Bora, Serikali imetenga Sh bilioni 579.4 kwa ajili ya kuimarisha utawala bora, ikiwa ni pamoja na kugharimia Bunge Maalumu la Katiba; vitambulisho vya Taifa; Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2014; kuhuisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura; maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015; mapambano dhidi ya rushwa na utoaji wa haki kwa wakati.

Katika jitihada za kuongeza mapato zaidi, Waziri wa Fedha ameondolewa mamlaka ya kusamehe kodi katika maeneo muhimu, ambapo Waziri Mkuya aliwaomba wabunge waiunge mkono Serikali, katika hilo ili kurahisisha usimamizi wa kodi nchini na hivyo kutoa unafuu kwa walipa kodi, na kuongeza mapato ya Serikali.

“Serikali itachukua hatua kuu mbili muhimu. Kwanza, kutoa taarifa ya misamaha ya kodi kila robo mwaka kwa kuwatangaza walionufaika na misamaha kwenye Tovuti ya Wizara ya Fedha.

“Hatua hii itasaidia kuleta uwazi na uwajibikaji katika suala la misamaha ya kodi na kuwafanya wananchi wajue ni nani anayenufaika na misamaha hiyo,” alisema.

Pili, alisema Serikali itatoa taarifa ya kina ya misamaha yote ya kodi iliyotolewa na kuiwasilisha bungeni kila mwaka, ili wabunge mpate nafasi ya kujadili na kutoa maoni yenu.

SHARE THIS POST TO SOCIAL MEDIA BELOW: