January 25, 2016

TRA Yadai Kukamata Simu 2,744 Katika Ghala la StarTimes zilizoingia Nchini Kwa Magumashi

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imedai kukamata maboksi 294 yenye simu 2,744, na vifaa mbalimbali vya simu katika ghala la Kampuni... thumbnail 1 summary


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imedai kukamata maboksi 294 yenye simu 2,744, na vifaa mbalimbali vya simu katika ghala la Kampuni ya StarTimes.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya StarTimes, Clement Mshana alisema yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa wiki na hajapokea taarifa yoyote kutoka TRA kuhusu kukamatwa kwa mizigo hiyo.

“Nimesikia kwenye gazeti lenu sijui chochote,” alisema.

Juzi, mamlaka hiyo ilikamata maboksi hayo ambayo thamani yake haijajulikana baada ya kutilia shaka nyaraka za mizigo hiyo iliyoingizwa nchini ikiwa haionyeshi ni ya nani.

Pia, TRA ilitilia shaka mizigo hiyo ilikotoka na kuwa na taarifa zenye utata kuhusu idadi ya mizigo hiyo. Mkurugenzi wa Huduma ya Elimu kwa Mlipa Kodi (TRA), Richard Kayombo alisema walipokea taarifa za utata wa mizigo iliyodaiwa kuingizwa na kampuni hiyo jambo lililowalazimu kwenda kuikamata kwa ajili ya uchunguzi.

“Tulikamata maboksi yaliyokuwa na simu na vifaa mbalimbali kama vile betri, chaji za simu, powerbank na kava za simu,” alisema Kayombo.

Alisema baada ya kuikamata waligundua kulikuwa na udanganyifu wa idadi ya maboksi yaliyokuwa kwenye nyaraka, kwani zilisomeka kuwa kuna maboksi 211, lakini katika uchunguzi walikuta 294.

Alisema mizigo hiyo ilikuwa haionyeshi ni ya nani na kama imelipiwa kodi, hivyo bado iko mikononi mwao hadi pale watakapojiridhisha na uchunguzi.

“Boksi hizo ziko chini ya TRA, bado tunaendelea na uchunguzi ili kujiridhisha na kujua mizigo hiyo ni ya thamani kiasi gani, imelipiwa kodi na kufuata taratibu zote za usafirishaji au la,” alisema.

Alisema endapo watabaini kuwa mizigo hiyo haijalipiwa kodi hatua za kisheri a zitachukuliwa kwa wahusika.

SHARE THIS POST TO SOCIAL MEDIA BELOW: