January 25, 2016

Kigogo Mwingine Akumbwa na Kasi ya Rais Magufuli, Kisa Rushwa

Rais John Pombe Magufuli  TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Katavi inamshikilia Ofisa Mtendaji wa Mtaa w... thumbnail 1 summary


Rais John Pombe Magufuli 
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Katavi inamshikilia Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Kawajense, Manispaa ya Mpanda Catherine Kipeta kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya Sh 30,000.

Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Katavi, Christopher Nakua alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 18, mwaka huu katika eneo la Mtaa wa Kawajense baada ya kuandaliwa mtego ambao ulifanikisha kukamatwa kwake.

Alisema mtuhumiwa alikamatwa kufuatia Ofisi ya Takukuru kupokea taarifa kutoka kwa mlalamikaji kuwa Ofisa Mtendaji huyo anamuomba rushwa kiasi cha Sh 30,000 ili asimpeleke kwenye Baraza la Kata kwa kosa la kufungua sehemu yake ya biashara wakati ni muda wa kufanya usafi na kutokushiriki kufanya usafi.

Ilidaiwa kuwa baada ya kupokea taarifa hizo ofisi ya Takukuru ilifanya uchunguzi na baada ya kuridhika na maneno ya mlalamikaji ndipo mtego ulipoandaliwa na mtuhumiwa kukamatwa.

Kamanda Nakua alisema mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma zinazomkabili ambazo ni kuomba rushwa ya fedha taslimu Sh 30,000, shtaka la pili litakuwa ni kupokea rushwa ya Sh 30,000 kinyume cha kifungu cha 15 (1) (a) cha sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa Na 11 ya mwaka 2007.

SHARE THIS POST TO SOCIAL MEDIA BELOW: