January 08, 2014

HOLLY SIN (DHAMBI TAKATIFU) - 2

ILIPOISHIA: “NAONA maisha ya hapa shuleni yamekuwa mazuri sana, mnakua vizuri kama mapacha,” alisema mzee Kenan na kuwafanya wawili h... thumbnail 1 summary

ILIPOISHIA:
“NAONA maisha ya hapa shuleni yamekuwa mazuri sana, mnakua vizuri kama mapacha,” alisema mzee Kenan na kuwafanya wawili hao wacheke kwa furaha.
Aidan akapakiza mizigo kwenye buti la gari na wakati akiendelea kufanya kazi hiyo, alichomoa diary yake aliyokuwa akitembea nayo mfukoni na kuichomeka kwenye begi la Caro bila mwenyewe kujua. Safari ya kurudi nyumbani ikaanza.

SASA ENDELEA…

WAKIWA njiani, Mzee Kenan alikuwa akiwatania mambo mbalimbali, hali iliyowafanya njia nzima wawe wanacheka kwa furaha. Baada ya muda, wakawasili mtaani kwao. Ilibidi wampitishe kwanza Carolina nyumbani kwao.
Gari liliposimama, Aidan ndiyo alikuwa wa kwanza kuteremka, akaenda kumsaidia Caro kuteremsha mizigo yake na kuiingiza ndani, wazazi wake wakatoka na kuwalaki wote wawili kwa furaha kubwa.
Baadaye, Aidan alirudi garini na kuondoka na baba yake mpaka nyumbani kwao ambako alipokelewa kwa furaha na mama yake. Baada ya kutumia muda mrefu kusalimiana na kusimuliana yaliyotokea wakati akiwa shuleni, baadaye Aidan alienda kuoga kisha akaingia chumbani kwake kupumzika.
Alipojilaza kitandani kwake, mawazo juu ya namna alivyokuwa akiteseka kwa penzi la Caro yalianza kujirudia ndani ya kichwa chake. Akawa anawaza mbinu nyingine atakayoitumia iwapo ile ya kumuwekea ‘diary’ kwenye begi lake itashindikana.
“Nitakunywa pombe ili kutoa aibu kisha nitamueleza ukweli,” aliwaza Aidan akiwa amelala pale kitandani, wazo hilo akaona litafaa zaidi kwani alishawahi kusikia kwamba mtu akinywa pombe, anakuwa hana aibu hivyo anaweza kuzungumza au kufanya chochote bila hofu.
Upande wa pili, baada ya Caro kusalimiana na wazazi wake na kusimuliana mambo mbalimbali yaliyotokea wakati akiwa shuleni, aliambiwa akaoge kisha apumzike kwani alionyesha kuchoka. Akaenda bafuni kuoga kisha akarudi chumbani kwake ambapo kabla ya kupumzika, aliamua kupanga vitu vyake vizuri.
Akafungua begi lake na kuanza kutoa nguo, vitabu, madaftari na vifaa vingine alivyotoka navyo shuleni. Wakati akiendelea na kazi hiyo, alishtuka kuona diary ambayo aliitambua haraka kuwa ni ya Aidan.
“Ooh! Amesahau diary yake, ngoja nikipumzika nitampelekea,” Caro alijisemea kisha akaiweka juu ya droo ya kitanda chake, akaendelea kutoa vitu vyote mpaka alipomaliza, akavipanga kila kimoja sehemu yake kisha akarudi kitandani na kujilaza.
Japokuwa alikuwa na uchovu, usingizi haukumjia haraka, akaanza kutafakari mambo mbalimbali aliyokutana nayo shuleni kwa kipindi chote alichokuwa masomoni.
“Hivi kwa nini siku hizi Aidan ananiangalia sana usoni na kunisifia kwamba mimi ni mzuri? Kwani nimebadilika nini?” alijiuliza Caro huku akisimama na kusogea kwenye ‘dressing table’ kubwa iliyokuwa ndani ya chumba chake, akaanza kujitazama kuanzia juu hadi chini, akawa anajigeuzageuza kama mwanamitindo, mwisho akaishia kutabasamu.
“Ana haki ya kunisifia, mimi ni mzuri kwelikweli,” alisema Caro na sura yake kupambwa na tabasamu pana, akawa anatembea taratibu kurudi kitandani kuendelea kupumzika.
Macho yake yakatua juu ya diary (kitabu cha kumbukumbu) ya Aidan iliyokuwa juu ya droo ya kitanda chake, akaitazama kwa muda kama anayejishauri kitu, akaamua kuachana nayo na kupanda kitandani, akaukumbatia mto wake na kuendelea kujigeuzageuza huku maneno ya Aidan kumsifia yakijirudiarudia kichwani mwake.
“Lakini hata yeye ni mzuri, mwili wake umejengeka vizuri na anavutia sana. Ngoja nimuandikie kwenye diary yake ili ije kuwa kama ‘sapraiz’ kwake siku akiiona,” aliwaza Caro na kuinuka, akachukua kalamu na ile diary ya Aidan, akarudi kitandani huku akiendelea kutabasamu, akaanza kuifungua.
“A diary of my love to Caro!” (Kitabu cha kumbukumbu za penzi langu kwa Caro!) ulisomeka ukurasa wa kwanza wa diary hiyo, moyo wa Caro ukalipuka na mapigo yake kuanza kumwenda mbio. Alirudia kuyasoma maandishi hayo zaidi ya mara tatu akihisi kwamba huenda amekosea kusoma lakini bado hali ilikuwa ni ileile.
Alishusha pumzi ndefu na kufungua ukurasa wa pili, alichokiona kilimfanya apigwe na butwaa akiwa ni kama hayaamini macho yake. Aidan alikuwa ameandika mambo mengi kuhusu yeye na Caro, akielezea ni jinsi gani alivyokuwa anampenda tangu wakiwa wadogo.
“Nilimpenda kama dada yangu na rafiki tangu tukiwa wadogo, lakini sasa nahisi mawazo yangu yanabadilika kwa kasi kila kukicha. Nataka awe mpenzi wangu lakini kumwambia siwezi, nitaendelea kuteseka…” ilisomeka sehemu ya maandishi aliyokuwa ameyaandika Aidan kwenye ukurasa huo.
Caro alifikicha macho yake akihisi huenda alikuwa ndotoni, akashusha tena pumzi ndefu na kuendelea kusoma. Alipomaliza alifungua ukurasa mwingine ambapo napo alikutana na maelezo marefu kutoka kwa Aidan akielezea jinsi alivyokuwa anampenda.
Aliandika mambo mengi ya kumsifia huku akijiwekea nadhiri kwamba siku atakayopata ujasiri, atamweleza ukweli unaomtesa ndani ya nafsi yake. Caro aliendelea kufunua ukurasa mmoja baada ya mwingine, akakutana na mashairi ya mapenzi, sifa kemkemu na kila aina ya maneno ya kimahaba, yote yakiwa yameandikwa na Aidan maalum kwa ajili yake.
Alijikuta akishindwa kujizua, machozi yakaanza kumlengalenga kwani ilionyesha dhahiri kwamba moto mkali wa mapenzi ulikuwa ukiwaka ndani ya mtima wake kiasi cha kumfanya ateseke sana. Alijilaza kitandani huku akiendelea kupitia kurasa za diary ile, machozi yakazidi kumtoka.
Licha ya kwamba alikuwa akimheshimu kama kaka na rafiki wa tangu utotoni, alijihisi mwenye hatia kubwa kwa kushindwa kuzielewa hisia za Aidan tangu mwanzo kiasi cha kumfanya ateseke kiasi hicho. Aliendelea kuwaza mpaka baadaye usingizi mzito ulipompitia.
Alipozinduka, tayari ilikuwa jioni, akili zake zikamtuma kujiandaa haraka na kumfuata Aidan nyumbani kwao kwani hakupenda kuendelea kumuona akiteseka kwa sababu yake. Akaingia bafuni kuoga kisha akarudi na kuanza kujipodoa. Alichagua gauni lake zuri lililomfanya aonekane mrembo mithili ya ndege tausi. Akaongeza bashasha kwa kujipulizia marashi mazuri ya kuvutia.
Alipohakikisha amependeza kisawasawa, alitoka kimyakimya bila hata kuaga na kwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa akina Aidan.
“Ooh! Karibu mrembo, karibu sana,” baba yake Aidan, mzee Kenan alimkaribisha Caro kwa bashasha, huku akiwa amevaa taulo tu. Ilionyesha kwamba alikuwa ametoka kuoga muda mfupi uliopita. Akamshika mkono na kuingia naye ndani.
“Mwenzako bado amepumzika, inaonyesha amechoka sana na mama yako ametoka kidogo, jisikie huru,” alisema mzee huyo kwa uchangamfu, huku akiwa amemkazia macho Caro hasa sehemu za usoni na kifuani mpaka msichana huyo mdogo akawa anajisikia aibu. Akawa anamwagia sifa kemkemu huku akijisogeza karibu naye.
Je, nini kitafuatia? Usikose kusoma hapo kesho ....

SHARE THIS POST TO SOCIAL MEDIA BELOW:

No comments