July 07, 2014

UNAZIJUA NUSU FAINALI TANO ZA KIHISTORIA KATIKA FAINALI ZA KOMBE LA DUNIA?

NUSU fainali ya kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil inaanza kesho. Hapa ni nusu fainali tano zilizochezwa na kuacha historia kubwa k... thumbnail 1 summary
Five memorable World Cup semi-finals
NUSU fainali ya kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil inaanza kesho. Hapa ni nusu fainali tano zilizochezwa na kuacha historia kubwa katika ulimwengu
wa soka.
1954-HUNGARY 4 URUGUAY 2.
Hii ndio nusu fainali inayosemwa kuwa kubwa zaidi katika michezo ya nusu fainali za kombe la dunia. Hungary iliyoiharibu Ujerumani Magharibi kwa mabao 8-3 katika mchezo wa makundi, iliongoza kwa mabao 2-0 dhidi ya mabingwa watetezi Uruguay mpaka dakika za mwisho na kuonekana inatinga fainali.
Lakini taifa hilo la Amerika kusini lilipambana kupitia kwa Juan Hohlberg aliyefunga mabao mawili na kuipeleka mechi katika dakika za nyongeza.
 Mabao mawili ya kichwa kupitia kwa Sandor Kocsic, aliyefunga mara 11 katika mashindano yote, yaliipa Hungary ushindi wa mabao 4-2. “Ilikuwa nusu fainali nzuri mno, ilikuwa mechi ya kasi, ufundi kwa timu zote”. Alisema nyota wa Hungary, Jozsek Boszik. Lakini walipoteza tena kwa mabao 3-2 dhidi ya Ujerumani Magharibi katika mechi ya fainali.
1966- ENGLAND 2 PORTUGAL 1
Ureno wakijivunia zaidi  nyota wao mkali `Black Panther` Eusebio katika fainali hizo walipoteza mchezo dhidi ya England. Mabao mawili ya Bobby Charlton yaliwafanya wenyeji waongoze kwa mabao 2-0 mpaka dakika 10 za mwisho.
Eusebio, aliyenyimwa nafasi za kufunga na kipa wa England, Gordon Banks kwa muda wote wa mchezo, alipata penati dakika ya 83 na kufunga. Hili lilikuwa bao la kwanza kwa England kufungwa katika mashindano hayo.
Licha ya kupata presha katika dakika za mwisho, England walifuzu fainali. “Kile kilikuwa kiwango kikubwa zaidi walichoonesha England mpaka leo hii,” alisema kocha Alf Ramsey. Wakati mpinzani wake, kocha wa Ureno, Otto Gloria alisema England itaifunga Ujerumani katika mchezo wa fainali kama itacheza soka kama lile. Ujerumani walitegemea sana soka la nguvu”. Alisema.
1970-ITALIA 4 UJERUMANI MAGHARIBI 3
Ukikumbuka mchezo huu wa karne ya 20, Italia walipata bao la kuongoza dakika nane tu za mchezo kupitia kwa Roberto Boninsegne na waliamua `kupaki` basi mpaka dakika ya mwisho ambapo Uwe Seeler alisawazisha.
Bao hilo liliupeleka mchezo katika dakika za nyongeza. Gerd `Der Bomber` Muller aliifungia Ujerumani bao la kuongoza, lakini Italia wakasawazisha, kabla ya kufunga bao la kuongoza kupitia kwa Luigi Riva.
Muller alifunga tena, lakini wakati Wajerumani wakiendelea kufurahia bao hilo, Italia walifunga bao la nne kupitia kwa Gianni Rivera na bao hilo likamaliza mchezo. Italia walicheza mpira mkubwa dhidi ya Brazil katika mchezo wa fainali, lakini walipoteza kwa mabao 4-1.
1980-UJERUMANI MAGHARIBI 3 UFARANSA 3 ( UJERUMANI WALISHINDA KWA PENATI 5-4).
Ilikuwa mechi ya maajabu. Ujerumani walifunga bao la kuongoza kupitia kwa Pierre Littbarski. Lakini Ufaransa walisawazisha kwa penati kupitia kwa Michel Platini. Muda wa nyongeza Ufaransa walifunga mabao mawili kupitia kwa Marius Tresor na Alain Giresse. Hata hivyo, Ujerumani walisawazisha na kuwa 3-3 kupitia kwa Karl-Heinz Rummenigge na Klaus Fischer. Maxime Bossis alikosa penati iliyookolewa na kipa Schumacher na Ujerumani kushinda kwa penati 5-4. Ufaransa walikuwa wabunifu, lakini Ujerumani walikuwa na nguvu.
1998-UFARANSA 2 CROATIA 1.

Wenyeji Ufaransa walikosolewa sana mpaka kufika hatua ya nusu fainali. Croatia wakishiriki fainali za kombe la dunia kwa mara ya kwanza baada kujitenga na Yugoskavia, walifunga bao la kuongoza dakika moja tu baada ya kipindi cha pili kuanza kupitia kwa Davor Suker. Hata hivyo, Ufaransa walisawazisha dakika moja baadaye kupitia kwa beki wake Lilian Thuram, hilo likiwa bao lake la kwanza katika soka la kimataifa. Thuram pia alifunga bao la pili, alipiga magoti na kushangilia sana. Kitu pekee cha huzuni katika mechi ile ilikuwa ni kitendo cha Slaven Bilic kupigwa kichwa na Laurent Blanc na kusababisha Blanc apate kadi nyekundu. Alikosa mechi ya fainali ambayo Ufaransa walishinda mabao 3-0 dhidi ya Brazil.

SHARE THIS POST TO SOCIAL MEDIA BELOW: