July 07, 2014

MKATABA WA GESI UMEVUJA: TANZANIA KUPOTEZA SHS 1.6 TRILIONI KWA MWAKA‏

  Zitto Kabwe, Mb Mkataba wa mgawanyo wa mapato yanayotokana na uzalishaji wa Gesi Asilia (PSA) kati ya Shirika la Mafuta Tanzania na Kam... thumbnail 1 summary
 Zitto Kabwe, Mb
Mkataba wa mgawanyo wa mapato yanayotokana na uzalishaji wa Gesi Asilia (PSA) kati ya Shirika la Mafuta Tanzania na Kampuni ya Mafuta ya Norway
umevujishwa (https://onedrive.live.com/view.aspx?cid=0EC42B180C06D0B8&resid=...).Toka Mkataba huo uvuje na kuanza mijadala kwenye mitandao ya kijamii, habari zake zimekuwa zinazimwa na hivyo kukosa kabisa mjadala mpana kitaifa na hasa kwa wananchi wenye rasilimali zao. Mwanzoni wengi wetu tulidhani (kwa makosa) kuwa tatizo la mkataba huu ni eneo la umiliki wa kampuni tu (shareholding) kulingana na namna ulivyowasilishwa, kumbe mgawanyo mzima wa mapato unakwenda kinyume na maelezo ya Serikali na TPDC kwa umma.
Mkataba uliovuja unaonyesha kwamba makubaliano ambayo Serikali imeingia na Wawekezaji hawa kutoka Norway yanaenda kinyume kabisa na mfano wa mkataba unaotakiwa kusainiwa (Model PSA). Kwa mujibu wa makala iliyoandikwa na jarida la mtandaoni ( http://africanarguments.org/2014/07/04/leaked-agreement-shows-tanza... ) Tanzania itapoteza zaidi ya shilingi 1.6 trilioni kila mwaka kulingana na viwango vya uzalishaji wa gesi asilia katika Kitalu namba 2. Kitalu hiki kinamilikiwa na Kampuni ya StatOil ya Norway na kampuni ya ExxonMobil ya Marekani. Norway ni nchi inayosifika duniani kwa kupambana na rushwa na kwa kutumia vizuri rasilimali yake ya mafuta.
Uchambuzi nilioufanya kulingana na viwango vya mgawo wa mapato kati ya ‘model’ PSA na mkataba huu unaonyesha kwamba Tanzania itapata mgawo kiduchu sana na kinyume na mgawo unavyopaswa kuwa. Mgawanyo ni  kama ifuatavyo katika majedwali hapa chini; Ikumbukwe kuwa mgawanyo huu hupatikana baada ya mwekezaji kuondoa gharama zake za uzalishaji, kinachobakia ndio hugawanywa kati ya mwekezaji na Tanzania.
Jedwali 1 Mkataba wa mgawanyo wa Mapato unaopaswa kutumiwa na TPDC (Model PSA) katika Mikataba na Wawekezaji
Viwango vya uzalishaji kila siku (MMscf per Day)
Mgawo wa TPDC (Profit Gas)
Mgawo wa Mwekezaji (Profit Gas)
0
249.999
50
50
250
499.999
55
45
500
749.999
60
40
750
999.999
65
35
1000
1249.999
70
30
1250
1499.999
75
25
1500
Above 1500
80
20
Jedwali 2 Mkataba wa mgawanyo wa Mapato kati ya TPDC na Statoil/ExxonMobil.
Viwango vya uzalishaji kila siku (MMscf per Day)
Mgawo wa TPDC (Profit Gas)
Mgawo wa Mwekezaji (Share of Profit Gas)
0
299.999
30
70
300
599.999
35
65
600
899.999
37.5
62.5
900
119.999
40
60
1200
1499.999
45
55
1500
Above 1500
50
50
Ukilinganisha majdwali haya utaona kwamba mgawanyo wa mapato utafaidisha zaidi kampuni ya StatOil na ni kinyume kabisa na mkataba unavyopaswa kuwa.
Wakati mgawo wa nusu kwa nusu upo katika uzalishaji wa chini kabisa kwenye ‘model PSA’, kwenye mkataba wa StatOil mgawo huo upo kwenye uzalishaji wa juu kabisa. Ukilinganisha mgawanyo huu wa mapato, iwapo kiwango cha ‘model PSA’ kingetumika Tanzania ingepata shilingi 1.6 trilioni zaidi ya kiwango itakachopata kwenye mkataba wa sasa uliovujishwa. Hii ni kutokana na Bei ambazo Shirika la Fedha la Kimataifa limeweka katika uchambuzi wake (https://www.imf.org/external/pubs/ft/scr/2014/cr14121.pdf ) kuhusu Gesi asilia ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Mwandishi Ben Taylor katika makala iliyotajwa hapo juu, kiwango cha mapato ambacho Kampuni ya StatOil ya Norway itajipatia kutokana na mkataba huu wa kinyonyaji, katika kipindi cha miaka 15 ya kuzalisha Gesi Asilia nchini itakuwa ni sawa sawa na misaada yote ambayo Tanzania imepata kutoka Norway toka Tanzania ipate uhuru wake mwaka 1961. Tangu Tanzania ipate Uhuru Norway imetoa misaada ya thamani ya $2.5 bilioni, wakati kwa mkataba huu na Kampuni ya StatOil ambayo inamilikiwa na Serikali ya Norway, kwa miaka 15 watapata $5.6 bilioni. Kwa hiyo kwa miaka 7 tu Norway itakuwa imerudisha misaada yote yake mara mbili zaidi!
Kuvuja kwa Mkataba huu kumesaidia sana kuona ukweli wa matamko ya viongozi wetu kuhusu ni namna gani Tanzania itafaidika na utajiri wake wa gesi. Kama kwa mkataba huu mmoja tu Taifa litapoteza matrilioni ya fedha kiasi hiki, ipoje hiyo mikataba mingine 29? Hivi sasa ugunduzi wa Gesi Asilia nchini ni lita za ujazo trilioni 51 ambayo ni sawa na mapipa bilioni 10 ya Mafuta. Katika Gesi Asilia yote iliyopatikana nchini, StatOil peke yao wana jumla ya lita za uzajo trilioni 20, sawa sawa na mapipa ya mafuta bilioni 4 (zaidi ya mafuta yaliyogunduliwa nchini Uganda na Ghana kwa pamoja). Hata hivyo utajiri wote huu utainufaisha zaidi Norway na Marekani kupitia makampuni yao kuliko watu wa Tanzania. Watanzania watabakia wanapewa misaada ya vyandarua na mataifa haya ilhali wanafaidi Gesi Asilia yetu.
Natoa wito kwa Wizara ya Nishati na Madini kutoa tamko kuhusu mkataba huu kati ya Shirika la TPDC na StatOil. Vile vile Kampuni hii ya StatOil kutoka nchi rafiki mkubwa wa Tanzania ina wajibu wa kutoa maelezo ya kina kuhusiana na mkataba huu. Serikali ieleze ni hatua gani inachukua kurekebisha Mkataba huu. StatOil nao waeleze watachukua hatua gani kuhakikisha wanaacha unyonyaji huu mkubwa na wa aibu kwa Taifa la Norway.
Sasa ni wakati mwafaka Watanzania kuweza kuona mikataba yote ya Gesi na Mafuta ambayo Serikali imeingia na Wawekezaji. Uwazi wa Mikataba sasa. Nimewahi kuandika huko nyuma (PRESS RELEASE: Contracts review is a publicity stunt and creation o... ) kwamba njia pekee ya Watanzania kufaidika na utajiri wa rasilimali zao ni kuhimiza uwazi wa Mikataba. Mkataba huu wa StatOil uliovujishwa uwe ni chachu ya kulazimisha Serikali na Makampuni kuweka mikataba yao wazi. Tuanze mashinikizo haya sasa kwa faida ya vizazi vijavyo.

SHARE THIS POST TO SOCIAL MEDIA BELOW: