January 17, 2014

Loga, Pluijm wasimamishwa kufundisha ligi kuu ...SOMA HAPA



Kocha mkuu wa Simba SC, Zdravko Logarusic.
Na Sweetbert Lukonge
CHAMA cha Makocha Tanzania (Tafca), kimesema makocha wa kigeni wakiwemo wale wa Simba na Yanga, hawatakaa kwenye mabenchi ya timu zao wakati wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha mkuu wa Yanga  SC, Hans van Der Pluijm.
Simba sasa inafundishwa na Zdravko Logarusic, raia wa Croatia na Yanga imempata Hans van Der Pluijm kutoka Uholanzi.
Tafca imelipitisha suala hilo na kusisitiza kama klabu hizo hazitawasilisha nyaraka zao na kuwasajili makocha hao katika chama hicho, basi hawataruhusiwa kabisa kukaa kwenye benchi wakati timu zao zinashiriki Ligi Kuu Bara.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nalo liliunga mkono na kusema walichosema Tafca ni cha kikanuni na kinapaswa kutekelezwa.
Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Tafca, Michael Bundala amesema wanachofanya ni kufuata kanuni zilizowekwa na TFF.
“Mzunguko wa pili unaanza Januari 25, kama Simba, Yanga na timu nyingine watakuwa hawajawasajili makocha wao, wasahau kuwatumia.
“Hatutakuwa na mzaha, hatuwezi kukubali washiriki katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara,” alisema Bundala.
Maana yake kama Simba watafanya uzembe, Logarusic ataishuhudia Simba akiwa jukwaani kama ilivyo kwa van der Pluijm na Yanga.
Bundala alisema kanuni ya 61 ya TFF inayozungumzia makocha wa ligi kuu, inasema ni lazima makocha wa kigeni wanaokuja kufanya kazi hapa nchini watambuliwe na Tafca kabla ya kuanza kufanya kazi zao.
“Safari hii hatutaki mchezo, tayari tumeshaiandikia barua TFF tukiitaka izingatie kanuni na taratibu zake ilizojiwekea kwa faida ya soka la Tanzania,” alisema Bundala na kuongeza:
“Mpaka sasa hakuna kocha yeyote wa kigeni anayetambuliwa na chama, hawataruhusiwa kufundisha timu hizo ligi itakapoanza.”
Kuhusiana na hilo, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alipoulizwa kama wameipata barua hiyo ya Tafca alisema:
“Bado hatujaiona hiyo barua, lakini suala hili ni la kikanuni, hivyo lazima litazingatiwa.”

SHARE THIS POST TO SOCIAL MEDIA BELOW:

No comments