January 11, 2014

Hadithi .... Mimba ya Jini -06

ILIPOISHIA: Mustafa alimchukua mkewe na kumrudisha ndani akiwa katika hali ileile ya kupoteza fahamu. Baada ya kumlaza kwenye kochi a... thumbnail 1 summary

ILIPOISHIA:
Mustafa alimchukua mkewe na kumrudisha ndani akiwa katika hali ileile ya kupoteza fahamu. Baada ya kumlaza kwenye kochi alichukua simu ili kuwasiliana na Shehna.
Alipochukua simu alikuta bado ipo hewani aliita.
“Haloo Shehna.”
“Abee Mustafa.”
“Tayari.”
“Kile kichupa cha manukato kipo?”
“Sijui.”

“Kiangalie kama kipo chukua maji kwenye sahani ya bati nyeupe kiweke kisha chukua maji yale mpake kichwani. Akiamka mpe anywe na mengine mpake tumboni.
SASA ENDELEA...
Mustafa alikwenda chumbani na kukikuta kichupa juu ya meza ya kujipodolea. Alikichukua na kwenda kwenye kabati na kuchukua sahani ya bati nyeupe ambayo aliiweka maji na kukiweka kile kichupa na kufanya maji yale kunukia.
Alifanya kama alivyoelekezwa kwa kumpa maji kichwani. Ghafla mkewe alifumbua macho.
“Husna,” alimwita kwa sauti ya chini.
“Abee mume wangu,” aliitika kwa sauti ya chini huku akipepesa macho.
“Vipi?”
“Safi,” alijibu kwa sauti ya chini huku akikaa kitako.
“Unajisikiaje?”
“Mmh! Sijambo.”
“Kwani ilikuwaje?”
“Yaani nilikuwa natoka chumbani ghafla nikaanza kujisikia vibaya..yaani vibaya sana. Nikapata wazo la kukupigia simu, nilijitahidi kukujulisha lakini ghafla kilikuja kiza kizito kilichoendelea sikujua.”
Mustafa alimpa maji anywe, lakini mkewe alihoji.
“Ya nini?”
“We kunywa.”
Mkewe alikunywa, yaliyobaki alimpaka tumboni.
“Mume wangu mbona sikuelewi?”
“Ndiyo tiba yako.”
“Kwa nini tusiende hospitali.”
“Shehna amekataa.”
“Alikuja.”
“Ndiyo,” Mustafa alimdanganya mkewe.
“Jamani mbona hakukaa ili nimuone, yaani yule dada anaonekana mwema sana. Kwani anasema hali hii inatokana na nini?”
“Mimba.”
“Mimbaa!” Husna alishtuka.
“Ndiyo, anasema imeingia kwa mtindo huo.”
“Ndiyo nasikia leo mimba ikiingia mara moja mtu unaona mabadiliko makali.”
“Basi mke wangu inaonekana mambo ya jana mimba imeingia.”
“Siwezi kuamini mpaka nikapime.”
“Duka la dawa lipo jirani kanunue kipimo.”
Snura alinyanyuka ili atoke nje, mara simu yake iliita. Alirudi kwenye kochi na kuichukua ilikuwa inatoka kwa Shehna.
“Asalam aleykum,” alipokea Husna.
“Waleykumu salam,” aliitikia Shehna kwa lafudhi ya mwambao.
“Niambie shoga yangu, yaani umeniudhi kweli.”
“Kwa nini tena shoga?”
“Yaani kumbe jana umekuja hata kusubiri tuonane?”
“Nilikuwa na haraka, la muhimu afya mengine majaaliwa tutaonana tu.”
“Naona umenipigia simu una lipi shoga yangu?”
“Vipi unaendeleaje?”
“Mmh! Namshukuru Mungu.”
“Mambo ya kawaida, siku zote mimba zina ujaji wake kwa vile ni mara ya kwanza lazima imekusumbua.”
“Shoga hii siyo mimba, mimba gani ya siku moja?”
“Husna acha ubishi, mimi ndiye najua.”
“Kwanza shoga, wewe ni nani mganga au ji..” Husna alikata maneno.
“Malizia tu si ulitaka kusema mimi jini siyo?”
“Hapana shoga.”
“Utanijua tu muda si mrefu kama mimi mtu, jini, mganga au mchawi,” Shehna alisema kwa sauti kali kidogo.
“Samahani shoga sikuwa na maana hiyo bali kukujua tu,” Husna alijitetea.
“Si nimekueleza utanijua wasiwasi wako nini.”
“Kuhusu ujauzito siwezi kuamini japokuwa nina dalili zote za ujauzito huenda ni malaria mi nataka kupima ili nihakikishe.”
“Husna naomba suala lako usichanganye na masuala ya kizungu,” Shehna alimpa onyo mke wa Mustafa.

SHARE THIS POST TO SOCIAL MEDIA BELOW:

No comments